Wanigeria hawatahitaji kibali maalum kupata visa ya Tanzania

HomeKitaifa

Wanigeria hawatahitaji kibali maalum kupata visa ya Tanzania

Idara ya Uhamiaji Tanzania imetangaza kuwa raia wa Nigeria wameondolewa rasmi katika utaratibu wa Visa Rejea (Referred Visa), hatua inayowaruhusu kufuata utaratibu wa kawaida wa maombi ya visa wanapotaka kusafiri kuja Tanzania.

Kwa mujibu wa Idara hiyo, mabadiliko hayo yamefanyika chini ya Tangazo la Serikali Na. 246 la mwaka 2026 na yameanza kutumika mara moja.

Hatua hiyo inawaruhusu wasafiri kutoka Nigeria kuomba visa ya Tanzania kupitia mfumo wa mtandao wa Uhamiaji au katika vituo maalum vya kuingilia nchini bila kupitia mchakato wa ziada wa kupata kibali uliokuwa ukihitajika awali.

Chini ya mfumo wa Referral Visa, waombaji walipaswa kuwasilisha maombi mapema na kusubiri idhini ya Uhamiaji kabla ya kusafiri, huku wakishauriwa kuanza mchakato huo angalau miezi miwili kabla ya safari.

Mabadiliko hayo yalitangazwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 25, 2026 na kusainiwa na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle.

error: Content is protected !!