Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema baadhi ya magari yanayosafirisha maiti kwenda mikoa mbalimbali nchini yanatumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha mirungi, bangi na skanka.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, amesema taarifa za kiintelijensia zimebaini kuwa baadhi ya magari yanayosafirisha maiti kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini, ikiwemo Kilimanjaro, Arusha na Tanga, yamekuwa yakihusishwa na usafirishaji wa dawa hizo.
Amesema magari hayo wakati mwingine husafirisha dawa za kulevya yakiwa njiani kwenda kwenye misiba au yanaporejea kutoka maeneo hayo.
Kauli hiyo imetolewa wakati DCEA ikitoa taarifa ya operesheni zilizofanyika kati ya Julai na Septemba 2026 katika mikoa 14, ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.


