Dar es Salaam na mikoa mingine kuna imani kuwa karanga mbichi, mihogo mibichi, nazi na supu ya pweza ni miongoni mwa vitafunwa vinavyoongeza nguvu za kiume.
Wanaume wengi wanaamini wakitumia vitafunwa hivyo nguvu zao zitaongezeka hatua inayosababisha wengi kutafuna mara kwa mara na wajasiriamali wengi kuuza barabarani na sehemu zingine mtaani na kujipatia soko haswa? Lakini unajua wataalamu wanasema hakuna ukweli wa moja kwa moja kuwa vinaongeza nguvu za kiume kutokana na kutofanyiwa utafiti wa kisayansi.
“Supu ya pweza pekee ndiyo yenye uwezo huo kwa kuwa kuna utafiti ulifanyika na ukadhibitisha kama inaongeza homoni za kiume,” amesema mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Tiba na Taaluma Mloganzila, Theresia Thomas. Amesema wanaokula mihogo na karanga mbichi nazi na vinginevyo bado hakuna utafiti wa moja kwa moja uliobaini kuwa vinaongeza homoni za kiume, “Hakuna utafiti unaoonyesha vitu hivyo vinaongeza homoni.”
Hata hivyo, amesema iwapo mwanaume atakunywa supu ya pweza na akashindwa kufuata ulaji sahihi, mtindo bora wa maisha ni kazi bure. “Kwa vitu kama hivyo inatakiwa kuwa mwendelezo wa ulaji wa mara kwa mara lakini afya nyingine kwa ujumla iwe sawasawa, lazima ale vyakula vinavyompa nguvu, na viambata vingine ambavyo vinapatikana ambavyo pia ni muhimu lazima kuwe na mchanganyiko wa vitu vingi.”
“Iwapo mwanaume tayari ana tatizo la nguvu za kiume, hata ale karanga, supu ya pweza haitamsaidia anatakiwa aonane na mtaalamu.