Utafiti: Wanaotumia plastiki hatarini kupata saratani na upungufu wa nguvu za kiume

HomeElimu

Utafiti: Wanaotumia plastiki hatarini kupata saratani na upungufu wa nguvu za kiume

 

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya na Tiba (CUHAs-Bugando) na Taasisi ya Taifa ya Tafiti za Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kituo cha Mwanza wamesema watu wanaotumia bidhaa za plastiki, ndala na nywele bandia wapo hatarini kupata madhara ya saratani na pia wanaume kupungukiwa nguvu za kiume.

Mkuu wa Idara ya Afya ya Mazingira na Afya ya Usalama kazini katika Kitivo cha Afya ya jamii CUHAs- Bugando, Dk Elias Nyanza alisema walifanya utafiti Ilemela jijini Mwanza kwa kuzungumza na watumiaji,vikundi vya kijamii katika halmashauri ya jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela.

“Tulitumia njia hizo za utafiti ili kupata uelewa wa ndani zaidi kuwa nini hasa kinatokea hususani ikizingatia kuna mahitaji na ongezeko kubwa sana la matukio ya saratani kwenye maeneo yetu,” alisema Dk Nyanza.

Dk. Nyanza alisema pia tafiti zingine zilizofanyika nchi mbalimbali zimeonesha kuwa plastiki na mabaki yake yanakuwa na kemikali ikiwemo Polyvinyl Chloride ambayo huzalisha kemikali aina ya Dioxin na kusema kwamba kemikali hiyo ina madhara kiafya ikiwemo kusababisha saratani mbalimbali.

“Kuna kemikali nyingine inaitwa Bisphenol A (BPA) na Bisphenol S (BPS), pamoja na kemikali nyingine aina ya Phthaletes ambazo hutumika katika kutengeneza bidhaa za plastiki ambazo zinapokutana na joto kali ama moto hutoka katika plastiki na kuingia kwenye vyakula na kwenye mazingira kwa ujumla,” alisema Dk Nyanza.

Pia alisema, kemikali hizo zimeonekana kusababisha saratani ya matiti endapo mtu atazipata kwa wingi mwilini na akasema kemikali aina ya BPA husababisha mvurugiko wa homoni mwilini na kuchochea saratani hiyo na saratani ya tezi dume.

 

 

 

 

 

 

error: Content is protected !!