Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Malawi inafuatilia taarifa kuhusu magari ya mizigo ya wasafirishaji wa Tanzania yaliyokwama nchini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio hilo limesababishwa na mgomo wa umoja wa madereva wa magari yanayosafirisha mizigo na mafuta nchini Malawi unaoishinikiza Serikali ya nchi yao kuwasaidia madereva kuongezwa mishahara, kupunguziwa kiwango cha fedha za kuhuisha hati za kusafiria na mahitaji yao mengine.
Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi umewatembelea na kuzungumza na madereva katika baadhi ya maeneo waliyokwama ikiwemo eneo la Kanengo mjini Lilongwe na kwamba madereva hao wako salama pamoja na mali zao.
Baada ya jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi kufuatilia suala hilo na mamlaka za Malawi, kwa sasa magari hayo yameruhusiwa kuendelea na safari ya kurejea nchini na jitihada zinaendelea ili kuhakikisha madereva hao wanakuwa salama.
Wizara pia imewashauri madereva kutoa taarifa rasmi ubalozini ili kupata msaada unaohitajika pale wanapopatwa na changamoto mbalimbali badala ya kutumia mitandao ya kijamii na kuzua taharuki.