Kiongozi wa zamani wa Simba ahukumiwa miezi sita

HomeMichezo

Kiongozi wa zamani wa Simba ahukumiwa miezi sita

Hukumu ya kesi ya viongozi wa zamani wa timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Evans Aveva (aliyekuwa Rais wa Simba) na Godfrey Nyage (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba) imetolewa leo.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba ambapo Evans Aveva amehukumiwa kifungo cha nje kwa miezi sita huku Godrfrey Nyange (Kaburu) akiachiwa huru baada ya kutokutwa na hatia.

Kesi ya msingi iliyokuwa ikiwakabili viongozi hao ni kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Hakimu Thomas Simba ameeleza kwamba, fedha za mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi  (Dola za kimarekani 300,000) zilikuwa zimeingizwa kwenye akaunti ya Klabu ya Simba kupitia benki ya CRDB lakini baadae zilitolewa na kwa maelekezo ya kamati tendaji.

Kamati tendaji ilidai kwamba fedha hizo zinakwenda kutumika kwa ajili ya ujenzi wa nyasi bandia kwenye uwanja wa Simba huko Bunju, lakini badala yake fedha ziliingizwa kwenye akaunti binafsi ya Aveva.

Hakimu Mkazi Mkuu amesema “Mahakama imejitosheleza kuwa ile fedha ilitakiwa ijenge nyasi bandia kwenye uwanja wa Bunju lakini haikufanyika hivyo matokeo yake zilienda kwenye akaunti binafsi ya Aveva,”

Kutokana na mashtaka hayo Nyange amekutwa hana hatia na Aveva amekutwa na hatia kwa kutumia nafasi yake vibaya kwa kuingiza fedha hizo kwenye akaunti binafsi ingawa hakuna wizi uliofanyika.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba amesema “Kumpeleka gerezani kwa maana kumfunga haitasaidia chochote kwani watakuwa wamemfunga mgonjwa ambaye utakuwa imesababisha usumbufu siyo kwa mshtakiwa bali hata magereza na jamii kwa ujumla. Hata ukimpiga faini kubwa bado haitasaidia chochote kwani asipolipa atalazimika kupelekwa gerezani hivyo adhabu pekee inayomfaa mahakama imeona atumikie kifungo cha nje miezi Sita na asifanye kosa lolote,”

Mahakama imetoa nafasi ya rufaa kwa yeyote ambaye hajaridhishwa na hukumu hiyo

error: Content is protected !!