Lissu: Mwenyekiti yuko wapi

HomeKitaifa

Lissu: Mwenyekiti yuko wapi

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Tundu Lissu ametua nchini, akitokea Ubelgiji alikokimbilia baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 huku akimuulizia aliko Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye alitajwa kuwepo kwenye orodha ya kumpokea katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Lissu amewasili leo Jumatano, Januari 25, 2023 na kupokewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika aliyeongoza na viongozi wa Kamati Kuu waliokwenda kumpokea uwanjani hapo.

Mara baada ya kutoka nje ya geti la kuwapokea wageni uwanjani hapo, Lissu alionekana kuwa mwenye furaha alisalimiana na viongozi kwa kuwashika mikono ghafla akauliza, ” Mwenyekiti (Mbowe)yupo wapi? Si mliniambia atakuwepo? Eeeeh.

Hata hivyo, Mnyika alionekana kutabasamu huku baadhi ya viongozi walisikika wakimwambia kwamba atakutana naye Temeke viwanja vya Bulyaga katika mkutano wa hadhara alioandaliwa na chama hicho.

Lissu aliondoka nchini kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana jijini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge.

Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma alipopatiwa matibabu ya awali na baadae kukimbiza jijini Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.

Januari 6,2018 alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi hadi Julai 27, 2020 aliporejea nchini na kuwania urais lakini alishindwa na mgombea wa CCM, John Magufuli.

Hata hivyo Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Lissu aliondoka nchini kwenda Ubelgiji kwa madai ya kutishiwa usalama wake.

error: Content is protected !!