Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamishna Jenerali wa Magereza Mzee Ramadhan Nyamka kwenda kufanya kazi kwa weledi na uadilifu huku akilinda haki za wananchi wote.
Amesema hayo wakati wa uapisho wa Kamishna Jenerali wa Magereza na Majaji uliofanyika leo Agosti 29,2022 Ikulu Chamwino, Dodoma.
“Nakutaka uende ukaiongoze taasisi hii kwa weledi mkubwa…taasisi hii iliacha njia, mliacha ile kazi ya msingi ya kurekebisha tabia za hawa watu (wafungwa) lakini pia kulinda haki zao wakiwa kule (gerezani). Wale ni binadamu kama binadamu wengine wanahitaji hewa safi, mavazi ya sare zao, wanatakiwa kupata chakula kizuri…kwahiyo nenda kalinde haki zao,” amesema Rais Samia.
Pia amemtaka aende kuhakikisha kwenye taasisi ya magereza kuna utawala bora na kushauri kama ikibidi wapelekwe mafunzoni.
Rais Samia amemuagiza kwenda kuhakikisha kwamba wanarekebisha tabia za wahalifu ili kuwafanya kutorejea tena gerezani baada ya kuachiwa.
Aidha, Rais Samia amemtaka Jenerali Mzee kwenda kusimamia vizuri matumizi ya fedha katika taasisi ya magereza.
“Nenda kasimamie matumizi ya fedha na uhakikishe fedha hizi zinakwenda kwenye magereza yote kwenda kutoa huduma,” amesema Rais Samia.