Maandalizi ya Ujenzi wa Bwawa la Farkwa yashika kasi

HomeKitaifa

Maandalizi ya Ujenzi wa Bwawa la Farkwa yashika kasi

Serikali ipo katika hatua za awali za ujenzi wa bwawa la Farkwa, mkoani Dodoma.

Wizara ya Maji kupitia Programu ya Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi na uboreshaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma ( DSRSWSP) kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeendesha zoezi la kuhamisha shule ya msingi Mombose na Bubutole katika eneo la ujenzi wa Bwawa la Farkwa Wilayani Chemba, Dodoma.

Zoezi limeendeshwa na kwa kushirikiana na mamlaka za serikali ya mitaa.

Walimu na wanafunzi katika shule hizo wamehamishiwa katika shule mpya ya Sankwaleto iliyopo katika kijiji kipya cha Sankwaleto kata ya Farkwa.

Mratibu wa Elimu Kata ya Farkwa, Bw. George Mlawa amesema hadi sasa walimu na wanafunzi wa shule zote wameshahamishiwa katika shule ya msingi Sankwaleto na zoezi linaloendelea ni kutoa mabati na mbao pamoja na ubomoaji wa majengo ya shule hizo.

Ameongeza kuwa jumla ya wanafunzi waliohamia katika shule ya msingi Sankwaleto ni 872 ambapo wanafunzi 449 wanatoka shule ya msingi Mombose na 423 kutoka shule ya msingi Bubutole, na walimu 10.

Hatua hii ni zoezi endelevu la Wizara ya Maji ili kuhakikisha eneo la ujenzi linakuwa tayari kwa kuanza utekelezaji.

Lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wa Jiji la Dodoma na miji ya Wilaya za Bahi, Chamwino na Bahi inaondokana na changamoto ya upungufu wa huduma ya majisafi.

error: Content is protected !!