Serikali imetangaza kupatikana kwa wawekezaji wataotekeleza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha chuma chenye thamani ya zaidi ya sh600 bilioni eneo la Nala, jijini Dodoma.
Mradi huo utatumia madini ya chuma yanayopatikana nchini, kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma na kuajiri zaidi ya watu 6,500 kwa kazi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, ukiwa ni matokeo ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Tanzania.
Aidha, alisema mradi huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha madini ya chuma yanachakatwa ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje.


