Mahakama yabariki ushindi wa Ruto

HomeKimataifa

Mahakama yabariki ushindi wa Ruto

Mahakama ya Juu ya Kenya leo imepitisha kwa kauli moja kuchaguliwa kwa Rais mteule William Ruto katika kura ya urais ya mwezi uliopita baada ya kutupilia mbali mapingamizi dhidi yake.

Ruto anatarajiwa kuapishwa Jumanne Septemba 13, 2022.

Jaji Mkuu, Martha Koome aliyekuwa akitangaza uamuzi huo leo Septemba 5, 2022 amesema Uchaguzi Mkuu ulikuwa halali na madai yaliyotolewa na aliyekuwa mgombea Urais wa muungano wa Azimio, Raila Odinga yamekosa ushahidi kubatilisha matokeo yaliyotangazwa na Tume huru ya Uchaguzi na mipaka (IEBC).

“Tunatangaza kuwa matokeo ya ushindi wa Rais mteule ni halali,” amesema Jaji Koome wakati akitangaza uamuzi wa mahakama leo.

Uamuzi huo umetokana na  jopo la majaji saba waliopitia maombi ya Odinga na makundi mengine ya watu binafsi ambao walikuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyotolewa na IEBC.

Odinga kupitia mawakili wake alidai kuwa matokeo ya kura ambayo yalionyesha ameshindwa kwa tofauti ndogo ya asilimia 2 ni “upotovu” na kuishutumu IEBC kwa jinsi ilvyoendesha zoezi uchaguzi huo.

Jaji Mkuu Koome akitoa muhtasari wa kesi hiyo amesema walalamikaji wameshindwa kutoa ushahidi kuthibitisha madai yao kuhusu upotoshwaji wa matokeo yaliyotangazwa.

“Tumegundua kuwa Rais mteule aliyetangazwa alipata asilimia 50 +1 ya kura zote zilizopigwa kwa mujibu wa kifungu cha 138.4 cha Katiba,” amesema Jaji Koome.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa mshindi wa urais Agosti 15 baada ya kupata kura milioni 7.17 sawa na asilimia 50.49 ya kura zote zilizopigwa huku mshindani wake Odinga akipata kura milioni 6.94.

Odinga na wenzake walikuwa wakilalamika kuwepo wa udukuzi katika mtandao wa IEBC, hitilafu ya vifaa vya uchaguzi, utimilifu wa teknolojia iliyotumika, tofauti kati ya fomu halisi za uchaguzi na zile zilizowasilishwa kwenye tume, sambamba na kuathiriwa kwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika maeneo ambayo uchaguzi ulihairishwa awali.

“Rais Mteule ataapishwa Jumanne ya kwanza kufuatia siku ya 14 baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais ikiwa hakuna ombi lililowasilishwa chini ya Kifungu cha 140; au siku 7 kufuatia tarehe ambayo mahakama itatoa uamuzi wa kutangaza uchaguzi kuwa halali, ikiwa ombi lolote limewasilishwa chini ya Kifungu cha 140,” inasomeka sehemu ya Katiba ya Kenya.

Ni mara ya tatu tangu kuundwa kwake chini ya Katiba ya Kenya ya 2010 kwa mahakama hiyo kutoa uamuzi kuhusu mizozo na kesi za uchaguzi, kesi nyingine ziliwasilishwa mwaka 2013 na 2017.

Muda mfupi baada ya kutolewa kwa uamuzi wa mahakama, Rais mteule Ruto katika ukurasa wake ameandika, “ kwa wanadamu haiwezekani lakini kwa Mungu yote yanawezekana.”

error: Content is protected !!