Majaji walioweka historia Ikulu mpya Chamwino

HomeKitaifa

Majaji walioweka historia Ikulu mpya Chamwino

Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu Ikulu mpya ya Tanzania kuzinduliwa, leo majaji sita wa Mahakama ya Rufani wamekuwa watu wa kwanza kuapa katika jengo la Ikulu hiyo iliyopo mkoani Dodoma.

Mara tu baada ya uamuzi wa Serikali kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Tanzania mwaka 1973 mpango ulikuwa ni kujenga Ikulu ndani ya miaka 10.

Hata hivyo, safari hiyo haikutimia ndani ya muda uliopangwa hadi Mei 20, 2023 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua Ikulu mpya na ya kisasa ya Chamwino ikiwa ni miaka 50 tangu uamuzi wa kuhamia Dodoma kufanyika.

Mchakato huo wa ujenzi wa ikulu mpya ya Tanzania ulianza wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kuendelezwa na Marais wa awamu zote zilizopita na kukamilishwa na Rais Samia.

Historia imeandikwa tena katika Ikulu hiyo mpya ambapo majaji sita wa Mahakama ya Rufani wamekuwa watumishi wa umma wa kwanza kuapa katika jengo hilo.

Majaji hao ni Zainab Goronya Muruke, Leila Edith Mgonya, Amour Said Khamis na Dk Benhaji Shaaban Masoud. Wengine ni Jaji Gerson John Mdemu na Jaji Agnes Zephania Mgeyekwa.

Mwingine ni Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Tanzania Jaji mstaafu Rose Aggrey Teemba.

Mara baada ya kuapa, Rais Samia amewaambia kuwa wameweka historia kuapa katika Ikulu hiyo.

“Karibuni Ikulu mpya na hongereni kwa kuweka historia. Ndio wa mwanza kuapa hapa, nadhani kila mtu akipata picha yake atasema nikiwa jaji wa kwanza wa mahakama kuapa Ikulu mpya muweke wajukuu waje waione,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!