Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo kwa watu wanaotoa maneno ya uchochezi na kupotosha kuhusiana na suala la kuwahamisha wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro.
Waziri Majaliwa aliyasema hayo jana alipotembelea Kijiji cha Msomera kukagua ujenzi wa nyumba za wnaanchi waliokubali kuhama Ngorongoro.
“Haki zote za kibinadamu zimezingatiwa, na serikali itatoa usafiri wa wananchi na mizigo yao kutoka Ngorongoro mpaka hapa, pia tutalipa fidia kwa watakaohama baada ya nyumba zao kufanyiwa tathmini.” Waziri Mkuu.
Pamoja na hayo Waziri Mkuu alisema serikali itatoa ekari nane kwa kila mwananchi, ekari tatu kwa ajili ya makazi na ekari tano kwa ajili ya kilimo na kila mmoja apate maeneo ya uhakika na kutopata usumbufu.
Nae Naibu Waziri wa Ardhi, Ridhiwani Kikwete aliwataka wananchi wanaohamia Msomera kuhakikisha wanazingatia matumizi bora ya ardhi yaliyopangwa kwenye eneo hilo, ili kuepuka kutokea migogoro ya ardhi hapo baadaye.
Aliongezea kwa kuwataka maeneo yaliyojengwa kwa ajili ya josho na malisho ya mifugo yasiguswe.