Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kulivunja Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa sasa kwani suala hilo linagusa usalama wa nchi, kauli hii ameitoa jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
“Shirika letu la umeme nchini linafanya kazi kubwa. Linazalisha,linasafirisha na linagawa umeme kwenye maeneo mbalimbali nchi. Unapotaka kufanya jukumu la aina hii pia tuangalie sana usalama wa nchi,”
“Inabidi tuangalie kwa makini hasa unaweza kukatakata kwa kuwapa watu tofauti tofauti inaweza kutuletea athari kama nchi pale ambapo nchi mnahitaji umeme kwa wakati wote halafu mmoja miongoni wao akafanya tofauti kwa sababu zake itakuwa shida, ila tumepokea ushauri wako(Tarimba).” alisema Majaliwa.
Aidha , Majaliwa alieleza mpango wa usambazaji wa umeme vijijini na kusema kuwa mkakati wa Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inapeleka umeme kwenye vijiji vyote ifikapo Desemba, mwaka huu.