Makamba atoa majibu kamili bei ya mafuta

HomeBiashara

Makamba atoa majibu kamili bei ya mafuta

Waziri wa Nishati, January Makamba ametoa majibu kuhusu bei ya mafuta nchini kama ambavyo bunge lilimuagiza juma lililopita kuja na majibu ya hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na changamoto hiyo inayoikumba dunia.

Akitoa majibu mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. January Makamba alifafanua hatua za kifedha na zisizo za kifedha zilizochukuliwa na serikali.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe shilingi bilioni mia moja (Shilingi 100,000,000,000) kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini.

“Ruzuku hii ya shilingi bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia tarehe 1 Juni 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa,” alieleza Waziri Makamba.

Kuhusu hatua zisizo za kifedha zilizochukuliwa na zinazotarajiwa kuchukuliwa na serikali ni pamoja na, Kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund), Kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve), Kuwa na kituo kikubwa cha mafuta (Petroleum Hub), Kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi na Kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja). 

Aidha, Waziri Makamba alilieleza Bunge kwamba, ingawa tatizo hili la mafuta ni kwa dunia nzima, Tanzania tuna afadhali na akiba ya mafuta yatakayoweza kutosheleza mahitaji ya wananchi.

“Leo tunapozungumza tunayo petroli ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 34, dizeli ipo ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 27, mafuta ya taa kwa siku 81 na mafuta ya ndege kwa siku 26. Haya ni mafanikio kwani sote tunafahamu kwamba zipo nchi zimelazimika kutaifisha mafuta ya nchi nyingine yanayopitia kwao kutokana na uhaba wa mafuta.” alieleza Waziri Makamba.

 

 

error: Content is protected !!