Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amefanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Mto Ng’ombe, Tandale, Dar es Salaam, kukagua hali ya usafi wa mazingira na maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Waziri wa TAMISEMI pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni, Ndejembi ameelekeza Mkoa huo kuhakikisha mto huo unasafishwa na taka zilizorundikana kandokando ya Mto Ng’ombe zinaondolewa haraka na mazingira yanaendelea kuwekwa katika hali ya usafi.
Aidha, amewaagiza viongozi wa Halmshauri, kupitia maafisa mazingira na maafisa maendeleo, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzingatia usafi na ukusanyaji wa taka. Amesema ni muhimu kwa Halmashauri kuweka miundombinu mizuri ya kukusanya taka na kuzichukua kwa wakati ili wananchi wasitupe taka hizo katika maeneo yasiyofaa.
Vilevile, ameelekeza mamlaka za Wilaya ya Kinondoni kuweka utaratibu wa maeneo rasmi ya kutupa taka ili wananchi wawe na sehemu zinazotambulika kwa ajili ya kuhifadhi taka, hatua itakayosaidia kudhibiti utupaji holela na uchafuzi wa mazingira.


