1. Urafiki wa jinsia tofauti
Kama mwanandoa una tatizo linalokusibu, unapotafuta mtu wa kukushauri, hakikisha anakuwa labda kiongozi wa kiroho au tabibu wa masuala ya akili. Uzoefu unaonesha kuwa kumueleza mtu hisia zako mara nyingi huzalisha huruma, huruma huzalisha hisia za mapenzi na hatimaye mnaweza kujikuta mnaingia faragha zaidi kutimiza mahitaji ya hisia zenu za miili.
2. Usipende kumkosoa kila kitu mpenzi wako
Ukiwa mbele za watu na mkeo au mumeo hakikisha unamuunga mkono kila anachosema kama atakutaka au kukuonesha ishara ya kufanya hivyo. Ukipenda kukosoa sana, mpenzi wako ataanza kukuepuka kwa hofu ya kwamba utamkosoa. Mtu anaweza kushindwa kusema kitu au kutoa ushauri fulani ambao ungekuwa na tija kwenye maisha yenu, kwa hofu tu kukosolewa.
3. Tabia ya kupenda kushuku mambo au kujishuku kupita kiasi
Kuna watu wanatabia ya kushuku na kuhukumu bila kufanya uchunguzi, mwisho wa siku wanakuja kugundua mashaka yake hayakuwa ya kweli hata kidogo, aibu na haya huwatawala. Kupenda sana kujishuku au kushuku mambo ni moja ya dalili za kutokujiamini au kutokumwamini mwenza wako.
4. Mashemeji na mawifi
Hawa sio watu wabaya katu, kimsingi hakuna mtu mbaya kwenye familia, tatizo tunashindwa kuweka mipaka. Ni kweli mke na mume kila mmoja ana namna alivyolelewa nyumbani kwao na aina ya mahusiano aliyokuwa nayo na ndugu zake. Uhusiano huu ni lazima udhibitiwe mmoja wenu aingiapo kwenye ndoa, dada yako au kaka yako asiwe dereva wa maamuzi ya ndoa yako.
5. Tabia ya kupenda kupuuza mambo
“Ziba Ufa Usijenge Ukuta”.. ukifanya kosa hata ukihisi ni dogo, kuwa muungwana kuomba radhi. Mlundikano huo wa maudhi baada ya muda unakomaa na kuwa kama bomu la majira, linasubiri tu muda ufike lilipuke. Kuziba nyufa ni kuomba radhi punde tu makosa yanapotokea.