Mambo yakufanya kama hautahesabiwa

HomeKitaifa

Mambo yakufanya kama hautahesabiwa

Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao hawajahesabiwa na unafikiri unaweza usipate fursa hiyo katika muda uliopangwa wa siku saba, ondoa shaka maana kila mtu atafikiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Zoezi la hilo linalolenga kupata taarifa na data muhimu kuhusu watu  na makazi lilizinduliwa Agosti 23, 2022 na linatarajiwa kuendelea hadi Agosti 29 mwaka huu Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam juzi Agosti 24 amesema amewaelekeza waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya kuandaa namba maalum itakayotumika na watakaokuwa hawajahesabiwa baada ya Agosti 29.

Hatua hiyo itasaidia wananchi ambao hawajahesabiwa kufikiwa katika maeneo yao na kutimiza wajibu wa kuhesabiwa.

“Napenda pia kutoa wito kwa waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa wanaandaa utaratibu wa kuwa na namba rasmi ya simu ambayo wananchi wataitumia kupiga simu kama watakuwa bado hajahesabiwa baada ya tarehe 29 Agosti, 2022 ili utaratibu maalum uwekwe wa kuwafikia,” amesema Makinda.

Licha ya kuandaliwa kwa namba maalum zitakazotumika kutolea taarifa kwa kaya ambazo zitakuwa hazijahesabiwa ndani ya siku saba, pia wameshauriwa kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo husika.

“Wananchi wanapaswa pia kutoa taarifa kwa kiongozi wa eneo lake ambaye ana mawasiliano na karani wa sensa ili aweze kujulishwa na hatimaye ahesabiwe,” amesema Makinda.

Aidha, kutokana na kuibuka kwa  migogoro ya mipaka katika baadhi ya maeneo wakati wa  Sensa,  Makinda amesema zoezi la Sensa  halina mamlaka ya kurekebisha mipaka hivyo  wananchi wa maeneo hayo washiriki zoezi hilo kikamilifu huku mamlaka husika zikishughulikia changamoto hizo.

Kwa mujibu Mfumo wa ufuatiliaji wa ukusanyaji wa taarifa za Sensa, asilimia 17.13 ya kaya zote nchini zimehesabiwa ndani ya siku moja Agosti 23 kwenye Sensa ya Watu na Makazi.

Lengo kwa siku ya kwanza lilikuwa kufikia asilimia 15 ya kaya lakini wamevuka hadi asilimia 17.13 huku Makinda akisema hayo ni mafanikio makubwa ya zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Kamisaa huyo wa Sensa,  siyo watu wote wangeweza kuhesabiwa kwa siku moja ndiyo maana zimewekwa siku saba kukamilisha zoezi hilo.

Wananchi ambao bado hawajafikiwa na makarani wa Sensa wametakiwa kuwa wavumilivu na kutoa ushirikiano ili kukamilisha zoezi hilo muhimu kwa maendelea ya Taifa.

error: Content is protected !!