Kampuni ya Apple itazindua simu mpya ya iPhone 14 mapema mwezi ujao ambayo inatajiwa kuja na mambo mbalimbali mazuri ikiwemo kuboresho muundo na kamera yenye uwezo wa kupiga picha zenye ubora wa hali ya juu.
Awali kampuni hiyo ya Marekani ilitarajia kuzindua simu hiyo Oktoba 2022 lakini imesema itafanya uzinduzi huo Septemba 7 mwaka huu na itaanza kuuzwa Septemba 16.
Simu hizo zitakuwa katika matoleo manne tofauti yaani iPhone 14 ya inchi 6.1, iPhone 14 Max ya inchi 6.7, iPhone 14 Pro ya inchi 6.1, na iPhone 14 Pro Max ya inchi 6.7.
Pia uzinduzi huo utajumuisha pia kompyuta mpya (Mac), tableti za iPad na saa za Apple zenye utendaji mzru kuliko zilizotangulia.
Kuhusu simu za iPhone, kutakuwa na maboresho ya kamera ambapo kwa sasa itakuwa pana zaidi ili kumuwezesha mtumiaji kupata picha kwa mapana na kuna uwezekano kwamba Apple itaanzisha lensi ya kukuza (periscope) ambayo itaruhusu kipengele cha “zoom” kupata picha kwa uzuri zaidi..
Pia katika simu hizo kunatarajiwa kuwa kihisishi (sensor) kipya na kikubwa zaidi kwenye kamera kuu itakayokuwa na uwezo wa megapiskeli 48 l. Sensor hii inatarajiwa kupamba thamani ya kiwango cha juu cha iPhone 14 Pro na Pro Max.
Hii itakuwa sensor kubwa zaidi ya kamera kuwahi kuwekwa kwenye matoleo ya simu za iPhone tangu zianze kutengenezwa.
Muonekano mpya
Simu za iPhone zitakazozinduliwa mwezi ujao, zitakuja na muonekano mpya ambapo iPhone 14 Pro na Pro Max zitakuwa na muundo wa shimo na kidonge ili kuwezesha kamera ya mbele kutambua sura ya mmiliki ili kuimarisha ulinzi wa simu hizo.
Apple inatarajiwa kupandisha bei ya simu za iPhone 14 Pro na iPhone 14 Pro Max kwa Dola za Marekani 100 sawa na Sh223,000 kutoka toleo la awali la iPhone 13.
Hiyo ina maana kuwa iPhone 14 Pro itauzwa kwa wastani wa Sh2.7 milioni kutoka sh Sh2.5 milioni ya iPhone 13 Pro.
Hata hivyo, matoleo mengine mawili ya iPhone 14 yanatarajiwa kutokuwa na ongezeko kubwa la bei, ili kuwapa unafuu watumiaji kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.