Matano aliyoongea Gerson Msigwa

HomeKitaifa

Matano aliyoongea Gerson Msigwa

Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo, Gerson Msigwa leo alioongea na waandishi wa habari jijini Dodoma. Katika mkutano huo, Msigwa alijielekeza kwenye kutoa taarifa juu ya shughuli za Serikali hadi kufikia mwezi Agosti 2021.

Click Habari inakuwekea mambo matano aliyozungumzia Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa katika mkutano huo na waandishi wa habari;

Maendeleo ya Bandari  

Gerson Msigwa amesema   “Katika miezi 6 iliyopita (Februari – Julai), bandari zetu zilizopo ukanda wa Bahari ya Hindi (Dar es Salaam, Tanga na Mtwara) na Bandari zilizopo katika maziwa yetu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) zimeongeza idadi ya meli zilizohudumiwa kutoka meli 1,388 (zilizohudumiwa katika kipindi hicho mwaka jana 2020) hadi kufikia meli 2,206. Halikadhalika kiwango cha shehena ya mizigo kimeongezeka kutoka tani Milioni 7.826 hadi kufikia tani Milioni 8.869.”

Msemaji Mkuu wa Serikali aliongelea maendeleo ya bandari katika maeneo yote ya nchi na kuonesha maendeleo chanya sambamba na mipango kabambe ya serikali katika kuboresha huduma katika bandari hizo.

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona (Uviko-19) 

Msigwa amesema mpaka sasa zaidi ya watu 300,000 (Laki tatu) wameshapata chanjo ya korona (UVIKO 19) huku Serikali ikiendelea kuwahimiza wananchi kuzingatia tahadhari zote za kujikinga dhidi ya huo.

Aliongeza… “Pia kulikuwa na malalamiko ya gharama za vipimo kwa wasafiri waendao nje ya nchi hasa kwenye viwanja vyetu vya ndege, lakini sasa tatizo limetatuliwa kwa kupunguza gharama za kipimo cha haraka kutoka Dola za Marekani 25 hadi 10, na kile kipimo kiitwacho PCR ambacho baadhi ya hudai kitumike kimepunguzwa kutoka Dola za Marekani 100 hadi 50”

Usafiri wa anga. 

Gerson Msigwa ameeleza kwamba Serikali imeshafanya malipo ya awali kwa ajili ya kununua ndege nyingine 5 ambazo zinatarajiwa kufika nchini mwaka 2023. Kwa upande wa huduma Msigwa amesema kwamba pamoja na kutoa huduma katika vituo 23 vya ndani na nje ya nchi, tayari Shirika  la ndege la ATCL limerejesha safari zake za kwenda India (zinaanza kesho), linasafirisha mizigo kwenda China na hivi karibu litaanza kwenda Nairobi, Kenya na Lubumbashi, DRC.

Ujenzi wa Reli (SGR). 

“Ujenzi unaendelea vizuri. Dar es Salaam –Morogoro tumefikia asilimia 93, na Morogoro Makutupora tumefikia asilimia 67.65 Mwishoni mwa Novemba mwaka huu tunatarajia kupokea Injini 2 na Mabehewa 12 ya treni ya majaribio katika njia yetu mpya ya SGR. Mabehewa mengine 18 yanatarajiwa kuwasili nchini ifikapo Juni 2022. Pia kuna mabehewa mengine 59 yatafika mwaka 2023.” alisema Gerson Msigwa.

Ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere katika mto Rufiji

Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa, ujenzi unaendelea vizuri na kwa sasa kazi zimefikia asilimia 57. Aliongeza kwamba kwa kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni mwakani, Serikali kupitia TANESCO inaendelea na manunuzi ya vifaa mbalimbali vikiwemo Transifoma, Mashine za kufulia umeme na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka ulipo mradi hadi Chalinze ambako itaungana na gridi ya Taifa.

Mengine aliyozungumzia Msigwa ni pamoja na suala la ukusanyaji wa mapato ambapo amesema Serikali inawapongeza Watanzania wote kwa kuitikia kulipa kodi bila shuruti, na inaendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji na ufanyaji biashara ili kodi iongezeke kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.

error: Content is protected !!