Matukio makubwa 10 yaliyotikisa Septemba 2021 nchini Tanzania

HomeMakala

Matukio makubwa 10 yaliyotikisa Septemba 2021 nchini Tanzania

Siku 30 za Septemba zimemalizika usiku wa kuamkoa leo. Katika saa 720 za mwezi huo, matukio mengi yametokea nchini kuanzia kwenye siasa, michezo hadi burudani. Wakati ukiinza Oktoba, tufanye mapitio kwa ufupi juu ya matukio 10 kati ya mengi yaliyotikisa zaidi Septemba.

Mpangilio wa matukio haya haujafuata umuhimu au ukubwa, au tarehe ya kutokea kwa tukio husika.

Tundu Lissu kufutiwa kesi
Septemba 22 mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilifuta kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleao (CHADEMA) Tanzania Bara, Tundu Lissu na wenzake watatu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Lissu na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002, katika kesi ya jinai namba 208/2016.

Kesi ya Ugaidi ya Mbowe
Kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Halfan Mbwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Ling’wenya inaendelea katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambapo sasa kinachosubiriwa ni hukumu ya kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi itakayotolewa Oktoba 19.

Katika kesi ndogo, Mbowe na wenzake wanapinga namna polisi walivyowahi na kuchukua maelezo, wakidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria. Katika kesi ya msingi washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili vitendo vya kigaidi.

Yanga kuondolewa Klabu Bingwa, Siku ya Wananchi, Simba Day, Kuanza Ligi
Waswahili husema “haikuwa riziki.” Yanga iliondolewa katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwenye hatua ya awali baada ya kufungwa 2-0 na Rivers United ya Nigeria. Lakini katika michezo matukio mengine yaliyosisimua ni Siku ya Mwananchi, ambapo Yanga ilifungwa 2-1 na Zanaco ya Zambia, Simba Day ambapo Simba ilifunga 1-0 na TP Mazembe ya DRC.

Nani anaweza kusahau mchezo wa Ngao ya Jamii, moja ya Derby kubwa Afrika iliyopigwa na Yanga wakaichabanga Simba 1-0, goli la dakika ya 11 la Fiston Mayele. Ligi nayo imeanza, baadhi zikianza vizuri kama Yanga, huku wengine wakichezea kichapo kama Ruvu Shooting au kugawana alama kama Simba.

Rais Samia kuhudhuria UNGA
Baada ya miaka 6, Tanzania iliwakilishwa tena kwenye Mkutano wa (76) wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Rais wa nchi. Hotuba aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo ni moja ya hotuba 10 bora zaidi kwa mujibu wa jarida la Foreign Policy.

Hotuba yake iligusia masuala kadhaa ikiwemo kuimarika kwa demokrasia na haki za binadamu nchini, kuboreshwa mazingira ya biashara na uwekezaji, chanjo ya UVIKO19 na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Rugemalira kuachiwa

Septemba 16 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimfutia mashtaka na kumwachia huru mfanyabiashara maarufu Tanzania, James Rugemalira. Hatua hiyo ilitokana na Mkurugenzi wa Mashataka nchini (DPP) kueleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo. Rugemalira ambaye alikuwa akishikiliwa tangu mwaka 2017, alikuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akituhumiwa kujipatia fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Uchaguzi 2025
Katika kuadhimisha siku ya Demokrasia duniani Septemba 15 Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na Wanawake Jijini Dare es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo moja ya jambo ambalo aligusia katika hotuba yake ni kuhusu mpango wa serikali katika kusaidia wanawake nchini, na pia akagusia umuhimi wa wanawake katika kuweka Serikali madarakani kwamba, kama wanawake watasimama nae hadi mwisho, baasi 2025 ni mwaka wa kumchagua Rais Mwanamke. Kuhusu baadhi ya vyombo vya habari kusema kuwa Rais Samia hatogombea 2025, alihoji “nani amewaambia?”

Ujauzito wa Vannessa Mdee
Vanessa Mdee, amekuwa akiishi Marekani na mpenzi wake Rotimi, mwigizaji na msanii wa muziki huyu kutoka Nigeria kwa kipindi kirefu sasa. Majumaa kadhaa yaliyopita Vanessa aliweka wazi kuhusu ujauzito wake. Habari hii ilipokelewa kwa hisia tofauti sana ukizingatia kuwa aliwashawahi kuwa na mahusiano na mwanamuziki mwenzake nchini Tanzania, Juma Jux, ambaye jamii ilimsakama kwa utani kuwa alishindwa kumpa Vanessa ujauzito. Hivi karibuni mwanamuziki huyo ameweka wazi kuwa amejifungua mtoto wa kiume ambaye wamempa jina ‘Seven.’

Mabadiliko ya Mawaziri
Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kurejea kutoa nchini Marekani alifanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake mawaziri. Katika mabadiliko hayo alimteua January Makamba kuwa Waziri wa Nishati, Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Prof. Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Kufariki Ole Nasha
Kifo cha Mbunge William Tate Ola Nasha ambaye pia alikuwa Naibu Waziri Ofisi wa Waziri Mkuu (Uwekezaji) kilichotekea tarehe 27 Septemba 2021 nyumbani kwake Jijini Dodoma kimepokewa kwa masikitiko makubwa na Serikali, watu wake wa karibu na Watanzania kwa ujumla.

Mo Dewjiu Kujiuzulu
Mwenyekiti na mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji almaarufu kama Mo Dewji ameamua kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC. Akitangaza uamuzi wake huo Septemba 29, 2021, Dewji amesema kwamba nafasi yake itashikiliwa na aliyekuwa Makamu wake, Salum Abdallah Muhene ‘Try Again.’

Je! Kwa upande wako, unadhani tukio lipi lilitikisa zaidi Septemba 2021?

error: Content is protected !!