Wizara ya Fedha na Mipango, imesema trilioni 2.4 zilizoidhinishwa na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ni kutokana na utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu ambapo zitatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kuleta nafuu kwenye mfumuko wa bei kwa kushusha bei ya mafuta na uchumi jumuishi.
Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, alisema fedha hizo zitatekeleza miradi ya kimkakati ambayo Rais Samia ameipa kipaumbele kwa manufaa ya wananchi.
“Tunashukuru IMF kwa kuidhinisha fedha ambazo zitaelekezwa kwenye kusisimua uchumi, huduma za kijamii,kuendeleza sekta binafsi. Tulikuwa na mjadala mkubwa sana na IMF hadi kufikia ukingoni sasa tutakwenda kupata Sh. trilioni 2.4 kwa maendeleo ya Watanzania,” alisema Mwaipaja.
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO), Gerson Msigwa, alisema fedha hizo zitaleta nafuu ya mfumo wa bei, mageuzi ya kiuchumi ili kuwa na uchumi jumuishi.
“Hizi ni fedha za masharti nafuu, zitasaidia kushusha bei ya mafuta, ruzuku ya pembejeo, kuwezesha vijana na makundi maalum. Haya ni matokeao ya dhamira njema ya serikali ya awamu ya sita, iko tayari kuendana na dunia,” alisema.
Msigwa alisema pia ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu nchini Marekani, ambaye alikutana na viongozi mbalimbali ikiwamo IMF ambao walituma timu kuangalia mahitaji ya nchi na andiko lake, na kwamba walifanya tathmini na kuona nchi inastahili fedha hizo.
Aidha, Naibu Mkurugenzi Mtendaji na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya IMF, Bo Li, alisema wameridhishwa na hatua za serikali ya Tanzania katika kupunguza matumizi na kuelekeza nguvu kuboresha huduma za kijamii kwa ufanisi kwa wananchi.
Pia, namna nchi ilivyoweka mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta na chakula, ambayo itaangaliwa katika kuangalia uhimilivu wa deni.