Mfalme wa Norway, Harald V amempongeza Rais Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba analinda na kuzipigania haki za mtoto wa kike nchini.
Pongezi hizo amezitoa jana Februari 13,2024 wakati wa Dhifa ya Kitaifa ambayo Mfalme Harald V wa Norway amemuandalia mgeni wake Rais Samia Suluhu.
“Wewe (Rais Samia Suluhu) una maarifa kwa unyenyekevu wako na utumishi kwa watu wako. Umefanya uongozi mzuri na kujitolea katika kuhakikisha kuwa sauti zote zinaweza kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sauti za wanawake na wasichana.” amesema Mfalme Harald V.
Katika hotuba yake, Mfalme Harald V amemuhakikishia Rais Samia ushirikiano katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu na pia kulinda haki zake za msingi.
“Kazi yako ya kuhakikisha haki ya elimu kwa wasichana ni ya kupongezwa. Tanzania na Norway wanashirikiana katika kujitolea kwa kulinda haki za wanawake na wasichana.” amesema Mfalme Harald V.
Ikumbukwe alipoingia madarakani, Rais Samia Suluhu aliruhusu wanafunzi waliopata mimba na wengine waliokatika masomo yao kwa sababu mbalimbali kurejea shule.