Tanzania na Norway kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo

HomeKitaifa

Tanzania na Norway kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo

Tanzania na Norway zimesaini Mkataba na Hati mbili za makubalino ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo.

Mkataba na Hati hizo zimesainiwa wakati wa Mkutano kuhusu Kilimo na Usalama wa Chakula uliofanyika katika Jengo la Climate jijini Oslo, Norway na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwanamfalme wa Norway Haakon.

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa hati hizo, Mhe. Dkt. Samia amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini hususan kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu akiwa madarakani, sekta ya kilimo nchini imendelea kukua na kuimarika ambapo kwa sasa Tanzania inajitosheleza kwa chakula na ziada ambayo wakulima wamekuwa wakiuza kwenye nchi jirani.

Mhe. Rais Samia ameongeza kusema jitihada zinafanyika ili uwepo wa chakula nchini usaidie kutokomeza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto wadogo hususan kwenye mikoa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa chakula.

Kadahalika amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wawekezaji ili kuhakikisha ardhi kubwa iliyopo nchini inayofaa kwa kilimo inatumika kuzalisha chakula cha kutosha na ziada.

Akizungumza kwenye mjadala kuhusu sekta ya killimo na mabadiliko ya tabianchi, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wadogo ambao ni asilimia 70, Serikali zinatakiwa kuwa na mfumo na sera madhubuti zitakazowawezesha wakulima hao kupata mitaji na teknolojia ili kujikwamua katika kilimo.

Pia ameongeza kusema ili wakulima hao wafaidike na kuona thamani halisi ya kazi yao ni vizuri kuwa na mifumo ya haki katika biashara ya mazao ya kilimo ili kumwezesha mkulima kunufaika.

Miongoni mwa Hati za Makubliano zilizosainiwa kati ya Tanzania na Norway ni kuhusu Ushirikiano wa Nchi Mbili katika Usalama wa Chakula na Kilimo.

error: Content is protected !!