Rais Samia awapongeza Ramadhan Brothers

HomeKitaifa

Rais Samia awapongeza Ramadhan Brothers

Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza vijana wa kitanzania wanaofahamika kwa jina maarufu la Ramadhan Brothers kwa kushinda shindano la ‘America Got Talent’ (AGT) ligi ya Fantasy.

Vijana hao wawili, Fadhili Ramadhani na Ibrahim Jobu wameshika nafasi ya kwanza katika fainali za shindano hilo zilizofanyika usiku wa Februari 19, 2024 na kuondoka na Dola za Marekani 250,000 sawa na Sh 637.3  milioni.

Baada ya ushindi wa kundi hilo kutangazwa, Rais Samia ametoa pongezi kwa vijana hao kupita kurasa za mitandao ya kijamii leo Februari 20, 2024 ambapo amesema ushindi huo unalitangaza vyema Taifa la Tanzania.

“Pongezi kwa vijana wetu Fadhili na Ibrahim (The Ramadhani Brothers) kwa kuibuka washindi katika mashindano ya sanaa na burudani ya AGT: Fantasy League…

…Safari yenu inaendelea kudhihirisha kuwa juhudi, nidhamu, kujituma na kujiamini ni nguzo muhimu kufikia mafanikio. Mnaitangaza vyema nchi yetu na kuweka mfano bora kwa wengine” amesema Rais Samia kupita ukurasa wa Twitter (X).

Akihojiwa na tovuti ya habari nchini Marekani US Today, Fadhili amesema wamefurahishwa na ushindi huo na anaamini maisha yao yataenda kubadilika.

“Tunaamni maisha yetu yatabadilika kuanzia sasa…hii ina maana kubwa sana kwetu tunafuraha sana hatuwezi kueleza,”amesema Fadhili.

Ushindi huo wa tuzo ya AGT ni matokeo ya jitihada zilizofanyika kwa zaidi ya miaka miwili ambazo hazikuzaa matunda waliyoyatarajia katika mashindano yamisimu iliyopita kupitia mchezo wa Sarakasi.

Mwaka 2023 majina ya vijana hao yalitajwa katika mashindano mengine ikiwemo Australia Got Talent ya Australia walikoishia nafasi ya tano na kupata hati ya dhahabu (golden buzzer).

Mengine ni pamoja na France Got talent ya Ufaransa pamoja na Romania Got talent ya nchini Romania.

Kutokana na kueperusha vyema bendera ya Tanzania vijana hawa pia walishawahi kupongezwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) hatua inayoashira kutambua mchango wao katika kuitangaza Tanzania kimataifa.

error: Content is protected !!