Mfumo mpya wa kodi kuanza Februari 9

HomeKitaifa

Mfumo mpya wa kodi kuanza Februari 9

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Februari 9, mwaka huu inatarajia kuanza rasmi matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) utakaokwenda kufanya kazi kwa saa 24.

Lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuwa na mfumo mmoja jumuishi ambao unalenga kwenda kusaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi na kulinda haki za walipakodi, kwani utasaidia katika utunzaji wa kumbukumbu. Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda ameeleza hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika wiki mbili, kuanzia jana hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mwenda amesema mfumo huo ni wa kisasa, utaongeza ufanisi, utaleta usawa na kuondoa usumbufu kwa sababu upatikanaji wa huduma utakuwa ni wa saa 24 katika siku saba za wiki ambao utafunguliwa Februari 6 na kuanza rasmi Februari 9, 2026.

Amesema pia utajumuisha huduma zote zilizokuwa zinatolewa katika mifumo ya TRA ikiwemo usajili wa walipakodi, utumiaji wa taarifa zote za kodi, ulipaji wa kodi, mawasiliano na madai mbalimbali kuendana na kauli ya mamlaka hiyo ya kwenda kuboresha huduma kwa walipakodi.

“Huu mfumo unakwenda kutenda haki kwa walipakodi, kwa sababu utakuwa na taarifa nyingi ambazo tutatoa makadirio sahihi lakini utaungana na mifumo mingine kwani ina uwezo wa kuungana na mifumo 500, kwa kuanza tutaanza na 60,” alisema Mwenda.

Ameongeza kuwa mfumo huo unakwenda kuwa njia kuu ya TRA kuwasiliana na walipakodi wao kwa kuwasilisha barua na kupokea majibu kupitia huko, pia umeungana na mfumo wa forodha ambao utaonesha kilichouzwa, kilichobaki na mapato yaliyopatikana.

Amesema pia utakuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu za walipakodi, kwani serikali imewekeza kwa ajili ya walipakodi, ikilenga kuwezesha biashara zao kwa kuwasaidia kutunza kumbukumbu ili wasiweze kuonewa na kugandamizwa.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yameanza na washauri wa kodi kwa sababu ndiyo watu wanaokwenda kuwafunza wateja wao, akiwasisitiza wakawe mabalozi wazuri kwa sababu katika mfumo huo mpya kuna fursa nyingi, ikiwemo kusafisha taarifa zao.

Sambamba na hayo, amesema uzinduzi wa mafunzo hayo unakwenda kufanyika katika mikoa 26 na watatoa mafunzo katika mikoa 33 ya kikodi nchini ili kuhakikisha kila mlipakodi anautambua mfumo huo.SOMA: TRA yaagizwa kukomesha matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi amesema mfumo mpya unashughulika na walipaji wa kodi za ndani na kusisitiza washauri wa kodi waliohudhuria kuufahamu, kwani ni jambo lisiloweza kuepukika ikiwa wanahitaji ufanisi.

Naye Mshauri wa Kodi, Victoria Soka ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi ili kuhakikisha huduma za kikodi zinaboreshwa kwa kurahisisha ulipaji wake. Amesema pia mfumo huo unawarahisishia kazi wao kama washauri wa kodi, kwani mtu anaweza kulipa akiwa mahali popote.

error: Content is protected !!