Mfumuko wa bei za vyakula kushuka Machi 2023

HomeKitaifa

Mfumuko wa bei za vyakula kushuka Machi 2023

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema kasi ya mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi inatarajia kupungua hadi asilimia 8.4 Machi mwaka huu kutokana hatua mbalimbali inazochukua Serikali ikiwemo kutoa ruzuku ya mbolea baada ya kupaa kwa kasi Disemba 2022.

Kasi hiyo, kwa mujibu wa Dk Chuwa huenda ikapungua kutoka asilimia 9.7 ya iliyorekodiwa Disemba 2022. Kiwango hicho cha Disemba mwaka jana kiliongezeka kutoka asilimia 9.5 iliyorekodiwa Novemba 2022. Mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji ulikuwa mara mbili ya wastani wa mfumuko wa bei wa kitaifa Desemba mwaka jana.

Dk Chuwa amewaambia wanahabari jana Januari 18, 2022 jijini Dar es Salaam kuwa mfumuko huo wa bei unaweza kushuka hadi kiwango hicho kutokana na vigezo mbalimbali ikiwemo kuanza kunyesha na kuimarika kwa msimu wa mvua katika maeneo mbalimbali.

“Kuanza kunyesha kwa mvua kama kulivyoripotiwa na TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania) kutasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima,” amesema Dk Chuwa wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo kuhusu mfumuko wa bei na uchumi.

Amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao kutasaidia kuongeza chakula sokoni katika msimu wa mavuno na hivyo huenda bei zikapungua na kuwaletea ahueni wananchi ambao wamekuwa wakilalamika ukali wa maisha.

Mtaalam huyo wa takwimu amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji pia ni kiashairia kingine ambacho wanafikiri kitachangia kupunguza mfumuko wa bei za vyakula.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya uchumi wamesema kupungua kwa mfumuko wa bei katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 kunategemea hali ya soko ya dunia ikiwemo bei za bidhaa muhimu kama mafuta ya kuendeshea vyombo vya moto.

“Kama bei ya bidhaa imepanda katika soko la dunia basi kuna uwezekano mkubwa ikapanda pia nchini. Kwa hiyo bei za soko hilo zina mchango katika mfumuko wa bei wa ndani,” amesema akiwemo Walter Nguma, mtaalamu wa masuala ya uchumi.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Suleiman Missango amesema kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua Serikali ikiwemo sera nzuri za kifedha, mfumuko wa bei nchini bado ni himilivu ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Desemba  2022 ulipungua kidogo hadi asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.9 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Novemba 2022 ikichagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za vyakula.

error: Content is protected !!