Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika kitaifa Julai 07, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 29, 2022 , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla, amesema kuwa, analishukuru Shirika la UNESCO nchini kwa kuendelea kuipa heshima lugha ya Kiswahili kwa kuadhimisha siku hiyo maalumu kila Julai 7.
“Maadhimisho haya kwa mwaka huu ni ya kipekee sana , tunatarajia kupata wageni wengi mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi, akiwemo Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe.Joachim Chisano, Rais Mstaafu wa Namibia Sam Nujoma, hii ni heshima kubwa kwa mkoa wetu ” alisema Makalla.
Ameongeza kwa kueleza kuwa, maadhimsho hayo yatahusisha shughuri mbalimbali ikiwemo kongamano kuhusu mchango wa lugha ya Kiswahili katika Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika, litakalofanyika Julai 06, 2022 ambapo Balozi Mstaafu Ame Mpungwe ataongoza mada mbalimbali.