Leo Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka mitatu madarakani akiwa kama Rais wa Tanzania baada ya kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli.
Dk. Magufuli aliaga dunia Machi 17,2021 katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam na akazikwa Machi 26 nyumbani kwake Chato mkoani Geita. Alizaliwa Chato Oktoba 29,1959.
Wakati akitangaza msiba huo, Makamu wa Rais wakati huo na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan alisema Dk Magufuli alifariki dunia kutokana na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.
Machi 19,2021, Samia aliapishwa katika Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Machi 22 wakati wa mazishi ya kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Rais Samia alisema Dk Magufuli alimuandaa vizuri kuongoza nchi hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi.
Alisema ataendeleza pale alipoishia Dk Magufuli na atahakikisha anafikisha nchi mahali alipotamani ifike.
“Tutahakikisha tunafanikisha na kufikisha Tanzania mahali alipotaka Tanzania ifike,” alisema Rais na kuongeza.
“Tumepikwa, tumeiva haswa na tumeiva sawa sawa, tupo tayari kuendeleza kazi alizoacha na kufikia pale alipotamani kufika kwa nguvu, kasi na ari ile ile.”
Miaka Mitatu bila Magufuli, kazi inaendelea
Anapotimiza miaka mitatu madarakani kama kiongozi mkuu wa nchi, Rais Samia amehakikisha Tanzania inapiga hatua na kupata maendeleo katika kila sekta. Aliwafuta machozi watanzania na kuwapa mwanzo mpya ambapo sasa dunia inashuhudia namna anavyoifanyia kazi kwa vitendo kauli yake ya KAZI IENDELEE.
Rais Samia amehakikisha kwamba kazi kweli inaendela huku wanaufaika wakubwa ni watanzania. Ameimarisha uchumi, ameboresha sekta ya afya na elimu, kilimo sasa ni cha kibishara zaidi na masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo yapo, ameimarisha mahusiano ya kimataifa na kurudisha Tanzania kwenye ramani ya dunia.
Kwa hayo machache ni dhahiri kwamba Rais Samia amedhamiria kusukuma gurudumu la maendeleo na Tanzania kuzidi kusonga mbele.