Neema kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2023

HomeKitaifa

Neema kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2023

Serikali imesema imefungua wigo kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2023 kubadili machaguo ya tahsusi ‘combinations’ ya kidato cha tano, kozi za vyuo vya ualimu, vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki ili kuwapa fursa wanafunzi kusoma masomo wanayoyapenda na yatakayowawezesha kujiajiri.

Taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa katika ofisi ndogo ya wizara, Kivukoni, Dar es Salaam imeeleza kuwa fursa hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na mitaala ya elimu kwa kidato cha tano.

“Utekelezaji huo umehusisha uanzishaji wa tahsusi mpya 49 kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahsusi 65,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amesema utekelezaji wa tahsusi mpya utaanza kutekelezwa kuanzia Julai 2024 zipo katika makundi saba.

“Tahsusi ya Sayansi ya jamii, Tahsusi ya Lugha, Tahsusi za Masomo ya biashara, Tahsusi za Sayansi, Tahsusi ya Michezo, Tahsusi za Sanaa na Tahsusi za Masomo ya dini,” amedadavua kiongozi huyo.

Amesema, kukamilika kwa zoezi hili kutatoa fursa kwa wanafunzi kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahsusi na kozi kwa njia ya mtandao ‘online’. Serikali itatumia kanzidata hiyo kuchagua wanafunzi watakaojiunga kidato cha tano na wale wa vyuo.

error: Content is protected !!