Rais Samia Suluhu Hassan amesema mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa barani Afrika unapaswa kuazimia kuongeza thamani ya zao hilo ili kufikia mwaka 2035 nusu ya mazao yatakayozalishwa yaongezewe thamani barani hapa.
Rais Samia amewasilisha azimio hilo baada ya kuonekana kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo barani Afrika kutoa asilimia 25 iliyokuwepo miaka ya 1960 hadi asilimia 11 miaka ya hivi karibuni.
Changamoto hiyo pamoja na nyinginezo kama kupanda na kushuka kwa bei pamoja na ufinyu wa biashara ya zao hilo kati ya nchi barani Afrika kumefanya zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya zao kunufaisha nchi nyingine duniani.

Rais Samia Suluhu Hassan(katikati) akinywa kahawa inayozalishwa nchini Tanzania na Waziri wa kilimo Hussein Bashe kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Barani Afrika (The 3rd G25 Africa Coffee Summit)
Akizungumza katika huo uliofanyika leo Februari 22, 2025 jijini Dar es Salaam amewataka wakuu wa nchi hizo kuazimia kuongeza thamani katika zao hili hilo ifikapo mwaka 2035.
“Nina amini jukwaa hili lilianzishwa kwa ajili ya kutuwezesha kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika sekta ya kahawa barani Afrika.
Kwa msingi huo napendekeza tuazimie kuwa ifikapo mwak 2035 nusu ya kahawa inayozalishwa Afrika iongezewe thamani hapa hapa afrika kabla ya kuuzwa ndani au nje ya Afrika,” amesema Rais Samia,

Rais Samia Suluhu akinywa Kahawa inayozalishwa nchini Tanzania wakati akiwahutubia Viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Barani Afrika.
Pamoja na azimio hilo kwa nchi zainazolisha kahawa Afrika, Tanzania imelenga kuongeza uzalishaji wa kahawa kufikia tani 300,000 ifikapo mwaka 2030 huku nusu ya mazao hayo yakiongezwa thamani nchini.
Kwa Mujibu wa Rais Samia kuongeza thamani kwa mazao hayo kutasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana wenye uwezo wa kufaya kazi ambao wamekuwa wahangaika kutafuta ajira.
Ili kuvutia vijana wengi zaidi katika sekta hiyo Rais Samia amewataka viongozi wa nchi zinazozalisha zao hilo kutengeneza mazingira rafiki yatakaoongeza ushiriki wa vijana katika kilimo.