Morogoro, Dodoma vinara ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa

HomeKitaifa

Morogoro, Dodoma vinara ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa

Tarehe 29 mwezi Septemba kila mwaka hutambulika kama Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani. Takwimu zilizotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk James Kihologwe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi zinaonesha kwamba kati ya Agosti mwaka huu watu 39,787 wameripotiwa kung’atwa na mbwa au wanyama wa jamii hiyo wenye kichaa.

Dk. Kihologwe amesema kwa Tanzania ugonjwa huo umeripotiwa kuwa na wagonjwa wengi kwenye mkoa wa Morogoro ambao kuna watu 4,329 huku Dododma ukishika nafasi ya pili kwa kuwa na wagonjwa 4,233.

Profesa Makubi amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa husababisha vifo na athari za kiuchumi kutokana na chanjo zake kuuzwa kwa gharama kubwa, pia aliongezea kwa kusema waathirika wakubwa wa ugonjwa huu ni watoto.

“Waathirika wakubwa wa ugonjwa huo ni watoto chini ya miaka 15 kutokana na ukweli kwamba ndio wanakuwa karibu na mbwa wanaofugwa na pia hupenda kucheza au kuchokoza mbwa wasiowajua,” amesema.

Ugonjwa huo hutokana kwa mnyama jamii ya mbwa hivyo kama mtu aking’atwa ni budi akaosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni halafu kidonda kisifungwe.

error: Content is protected !!