MovieFriday: Cryano

HomeBurudani

MovieFriday: Cryano

Filamu hii inaanza na mwanadada Roxane na unaweza kumwelezea binti huyo kama mwali anayevunja shingo za wanaume wote anaopishana nao. 

Relax, sio muuaji. Ninachojaribu kumaanisha ni kuwa, kwa jinsi wanavyogeuka kumtazama, lazima huwa wanalala na maumivu ya shingo.

Urembo wake unamweka kwenye darubini za watu wengi lakini kwa sasa, Roxanne, yupo kwenye kipindi cha mahusiano na De Guiche ambaye ni kamanda mkubwa kwenye jeshi la nchi waliyokuwa wakiishi.

Hata hivyo, De Guiche yupo kwenye mahusiano hayo peke yake kwani Roxane hata mpango na mwanaume huyo mwenye fedha zake.

Kwa maringo na mikogo ya Roxanne, unaweza kuhisi ni wa kishua au ana kila kitu lakini huwezi amini, na urembo wake wote alionao, anadaiwa kodi ya pango na kila siku anakimbizana na mwenye nyumba.

Kinachofikirisha zaidi ni kuwa, endapo akikubali tu kuolewa na De Guiche, huo utakuwa mwisho wa tabu zake zote duniani lakini Roxanne hafikirii hilo kabisa.

Roxanne ni mwanadada anayependa fasihi. Siyo kama binti wengi wanawaza mavazi, pesa, viatu, nguo na peremende. Yeye anafurahishwa na mwanaume ambaye moyo wake unanena zaidi ya mdomo.

Na ndiyo sababu ya kuwa na urafiki na Cyrano, jemedari wa jeshi la nchi hiyo ambaye amepigana vita vingi na kushinda.

Siku moja, Roxanne alikuwa anahudhuria michezo ya jukwaani yaani “plays” na huko alionana na kijana aliyeiba moyo wake. Ni Christian.

Kwa wadada hapa tutaelewana. Christian ni Mrefu, nywele zimekaa mahala pake, ngozi inateleza haswaa na sura yake unaweza kuifananisha na ya Josefu ambaye hadi mke wa Potifa alimdondokea.

Roxanne kwa kweli hakujali mahusiano yake na De Guiche kwani alichokihisi yeye ni “love at first sight”. Tukumbuke kuwa, Roxanne, ana mtu mmoja tu duniani ambaye ana uhakika wa neno “hapana” haliwezi kutoka kinywani kwake.

“Cyrano, naomba kuongea na wewe” Kijana Cyrano alihisi huo ni muda ambao Roxanne huenda ameelewa hisia zake na anataka kumjulisha kuwa naye anahisi hivyo hivyo.

Anayokutana nayo kwenye kikao hicho yanamvunja kwani ombi la Roxanne ni kumtaka ahakikishe kuwa Christian anakuwa mpenzi wake na anamuandikia barua kila siku.

Uso chini… tamaa iliyovunjika… moyo uliopasuka vipande vipande ndizo hisia za Cyrano.

Kwa kuwa hawezi kusema ndiyo, anakubaliana na ombi hilo na kuanza safari yake.

Uzuri wa Christian ni jambo moja lakini nilikwambia mwanzo kuwa Roxanne anapenda kuongeleshwa kwa moyo na siyo kinywa.

Pale Christian anapokutana na Cyrano, inakuja kwenye umakini wa Cyrano kuwa mtanashati huyo hajui chochote kinachohusiana na fasihi.

Maneno yake ni ya kawaida, barua zake haziwezi hata kumtoa mtu machozi kwa ufupi, barua yake ya kwanza kwa Roxanne huenda isingejibiwa kabisa.

Cyrano na Christian wanaamua kukubaliana. Kwa kuwa Christian naye anampenda Roxanne, anamruhusu Cyrano aandike barua zake. 

Barua moja inakuwa 50 na 50 zinakuwa 100 kwani wawili hao wanaandikiana haswa. 

Siku moja, Roxanne anaomba kukutana na Christian na wanapokutana, hapo ndipo taya zinapodondokea kwenye kifua.

Roxane anamwambia Christian amwabie maneno kama ambayo huyasema kwenye barua zake. Christian anasema yale yale, “Wewe ni mzuri kama ua” eheheheh,

Bwana bwana, nachoweza kukuibia siri hapa ni kuwa Roxanne alikasirishwa na hilo na kujiuliza yule ambaye alikuwa anaandika nakupenda kwa lugha ya moyo yuko wapi?

Nisimalize utamu wote. Tazama filamu hii kupitia majukwaa ya mtandaoni kujibu maswali yote unayojiuliza sasa.

Kutana na nyota wa filamu kubwa ikiwemo “Game of Thrones”, The Magnificent Seven” na nyingine kibao katika filamu hii.

Baada ya kuitazama filamu hii, huenda ukafunguka kwa mtu ambaye unampenda na usisubiri hata kesho.

error: Content is protected !!