Mpangaji amuua mwenye nyumba kisa kodi

HomeKitaifa

Mpangaji amuua mwenye nyumba kisa kodi

Mkulima wa Kijiji na Kata ya Likongowele, Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Siamini Mtopoka (40), anadaiwa kuuawa na mpangaji wake Shabani Matola kwa kukatwa na panga kichwani kwa kile kilichodaiwa ugomvi wa malipo ya kodi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walidai chanzo cha tukio hilo ni baba mwenye nyumba kufika alikokuwa anaishi mpangaji huyo kumdai malipo ya pango la nyumba. Walidai kuwa madai ya mmiliki huyo yalipingwa na mpangaji wake baada ya kumweleza kuwa kama nahitaji pango la nyumba yake, amlipe kwanza fedha alizokuwa anamdai kutokana na kazi aliyokuwa amempa ya kubangua korosho.

Mashuhuda hao walidai kauli iliyotolewa na mpangaji huyo haikumfurahisha mwenye nyumba ambaye alifunga mlango kwa nje na kuelekea Ofisi ya Ofisa Mtendaji Kata kwa lengo la kumshtaki mpangaji wake.

Walidai kuwa wakati akiwa njiani, mpangaji alivunja mlango, akatoka na kumfuata mwenye nyumba akiwa na panga mkononi na alipompata njiani alimpiga panga la kichwani akaanguka chini akafariki dunia papohapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Pili Mande, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa Shaban Matola amekamatwa na upepelezo ukikamilika atafikishwa mahakamani.

error: Content is protected !!