Bohari ya Dawa (MSD) imeingiza nchini shehena ya kwanza ya Naltrexone, dawa inayotumika katika matibabu ya uraibu wa pombe, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa watu wenye tatizo hilo.
Dawa hiyo imeingizwa kupitia ushirikiano kati ya MSD na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe katika juhudi za kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya zinazotumika kudhibiti uraibu wa pombe nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 23, 2026 na Meneja Mawasiliano wa MSD, Etty Kusiluka, usambazaji na uratibu wa dawa hiyo utasimamiwa na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.
Amesema MSD itaendelea kuingiza dawa hiyo kwa ajili ya taasisi hiyo ili kuhakikisha inapatikana kwa wagonjwa wanaohitaji huduma.
Naltrexone ni miongoni mwa dawa zinazotumika kutibu uraibu wa pombe na inaweza kusaidia kupunguza hamu ya kunywa kwa baadhi ya wagonjwa inapounganishwa na ushauri nasaha pamoja na huduma nyingine za kitabibu.


