Serikali imesema asilimia 14 ya fedha zinazotengwa kupitia Bima ya Afya kwa Wote zitaelekezwa katika kugharamia matibabu ya wananchi wenye magonjwa sugu, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wagonjwa wanaohitaji huduma za muda mrefu wanapata matibabu bila kukatishwa na changamoto za kifedha.
Amesema hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mkoani Dodoma.
Aidha, Dkt. Magembe amesema utekelezaji wa utaratibu huo unaenda sambamba na juhudi nyingine za Serikali za kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wanapata huduma za kibingwa, ikiwemo kutenga Shilingi bilioni tano kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya kibingwa.
Ameongeza kuwa Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu na kuhakikisha huduma zinazotolewa zina ubora unaostahili, bila kujali hali ya kiuchumi ya mwananchi.


