Muungano 2023 kusherekewa kipekee

HomeKitaifa

Muungano 2023 kusherekewa kipekee

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya  mwaka 2023 yatafanyika katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi tofauti ilivyozoeleka miaka ya nyuma.

Imezoeleka sherehe hizo kufanyika kitaifa kwa viongozi na wananchi kukusanyika uwanjani na kushuhudia shamrashamra mbalimbali ikiwemo haraiki ya watoto na glaride la majeshi.

Majaliwa ameyasema hayo leo Aprili 15, 2023 katika uzinduzi wa ripoti za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022, iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Tunguu.

Majaliwa amesema shughuli zitakazofanyika kwenye sherehe za maadhimisho ya mwaka huu ni pamoja na uzinduzi wa miradi ya maendeleo na utunzaji mazingira.

“Katika kipindi hiki cha maadhimisho kupitia mikoa, taasisi za Serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama yaambatane na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, shughuli za kijamii hususan upandaji wa miti, uchangiaji wa damu katika hospitali mbalimbali na vituo vya afya,” amesema Majaliwa.

Shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 17 hadi siku ya kilele Aprili 26, 2023 ni usafi wa mazingira, mashindano ya michezo, sanaa na uandishi pamoja na kampeni mbalimbali  za kupinga ukatili.

Sambamba na hayo Majaliwa ameagiza majengo yote ya Serikali kupambwa kwa mapambo na vitambaa vyenye rangi sahihi za bendera za Taifa na picha ya Rais wa Tanzania kwa Tanzania Bara.

“Kwa upande wa Zanzibar, majengo yote ya Serikali yapambwe kwa bendera sahihi ya Taifa na picha za waasisi wa muungano na picha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,” amesema Majaliwa.

Kila ifikapo April 26 Tanzania huadhimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yana kaulimbiu isemayo  “Umoja na Mshikamano Ndiyo Nguzo ya Kukuza Uchumi Wetu”.

Sherehe za maadhimisho kitaifa kufanyika 2024

Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amesema sherehe za kitaifa za  maadhimisho ya muungano yatafanyika mwaka 2024.

“Sherehe hizi zitafanya vizuri kitaifa itakapokuwa inakamilisha miaka 60, eneo la kufanyia shughuli hizo litajulishwa baadaye,” amesema Majaliwa.

Aidha Majaliwa amewaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kusimamia shughuli zote za sherehe za muungano kwa pande zote mbili yaani Tanzania bara na Zanzibar.

error: Content is protected !!