Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba amefafanua umuhimu wa mikopo katika nchi na kusema kila taifa lenye maendeleo lazima liwe na deni na kadri miradi mikubwa ya kimaendeleo inavyotekelezwa basi lazima deni lipande.
Mwigulu ameeleza kwamba mikopo hiyo mikubwa iliyochukuliwa na serikali ndio inasaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa na kurahisisha maisha akitolea mfano barabara nyingi zilizojengwa kuunganisha mikoa imekamilika kutokana na mikopo.
“Wakati mimi naanza first year (mwaka wa kwanza chuo) nchi nzima tulikua wanafunzi 2700 ndo watu walioenda chuo kikuu, tumetengeneza deni tukajenga UDOM(Chuoo Kikuu cha Dodoma) ndivyo ilivyo ni uamuzi,”- Waziri Mwigulu.
Aidha, Waziri Mwigulu amesema kwamba elimu itolewe kwa wananchi ili waweze kutambua namna ambavyo mikopo hii inachukuliwa na umuhimu wake katika nchi ili kuondoa dhana ya kwamba serikali inakopa sana hivyo kuhatarisha taifa.
“Wengine wakisikia hapa deni limeongezeka kwa asilimia 14.4 wanasema kwamba ina maana mwaka mmoja tu deni limeongezeka kwa trilioni 10,…niwaambie watanzania waelewe pia na kwenye hili deni la taifa ni tofauti ya fedha ya kwenye ATM. Deni ni mikataba iliyosainiwa,”- amesema Waziri Mwigulu.