Ngoma bado ngumu kesi ya Sabaya

HomeKitaifa

Ngoma bado ngumu kesi ya Sabaya

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita (Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya) imeahirishwa hadi kesho Novemba 24,2021.

Kubwa lililojiri Mahakamani leo hii wakati kesi hiyo ikisikilizwa, ni Mawakili wa Utetezi kuwasilisha pingamizi mahakamani wakipinga kupokelewa kwa nyaraka nne zilizoletwa kama sehemu ya ushahidi  na upande wa Jamhuri.

Shahidi wa 10 wa Jamhuri, mfanyabiashara Francis Mrosso (44) aliomba nyaraka nne ambazo ni leseni ya biashara, namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) na nyaraka mbili za usajili wa jina la kampuni yake ya Mrosso Injector Pump Service zipokelewe kama vielelezo.

Jopo la Mawakili wa Utetezi likiongozwa na Wakili Mahuna liliieleza mahakama kuwa wana sababu mbili za kisheria ambapo ya kwanza ni kuhusu nakala halisi ambazo ni TIN namba na leseni ya biashara na ya pili ni kuhusu nakala mbili za vyeti vya usajili wa jina la biashara ambazo siyo halisi hivyo kuomba mahakama isizipokee.

Kwa upande wao Mawakili wa Utetezi, walipinga hoja hizo za Utetezi kwa kusema kwamba nakala hizo ni halisi, na shahidi hakutakiwa kueleza namna alivyozipata nyaraka hizo katika hatua ya awali ya kuzikabidhi.

Shahidi huyo alieleza kwamba Sabaya aliwahi kufika katika eneo lake la biashara ambalo ni gereji ya Mrosoo Injector Pump Services akiwa na vijana wake ambapo walimshinikiza kuwapa fedha takriban milioni 10 ili wamlinde dhidi ya shutuma za kukwepa kodi.

Kesi hiyo ambayo inaendelea huku Sabaya akiwa kwenye kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, itaendelea tena kesho Novemba 24,2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

error: Content is protected !!