NIDA yawasihi wananchi kufuata vitambulisho vyao

HomeKitaifa

NIDA yawasihi wananchi kufuata vitambulisho vyao

Mamalaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imewataka wale wote ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao kwenda kwenye ofisi husika na kuchukua kwani hadi Desemba 31, 2021, zaidi ya vitambulisho milioni 1.1 vilikuwa bado vipo kwenye ofisi za serikali za mtaa, kata, shehia na ofisi za NIDA kutokana na wamiliki kutojitokeza kuvichukua.

Ofisa habari na msemaji wa NIDA, Geofrey Tengeneza aliwataka wananchi waliojiandikisha kwa vipindi tofauti kufika ofisi hizo kuchukua vitambulisho vyao kwani vipo tayari huku akitaja sababu moja wapo ya kuwepo kwa vitambulisho hivyo ni hamahama za watu.

“Kinachochangia kuwapo kwa vitambulisho vya watu katika ofisi hizo ni baadhi kuhama maeneo ya awali, kufariki, wengine wakishakuwa na namba ambayo wanaweza kuitumia katika kufanya kitu chochote anaona haina umuhimu kuchukua kitambulisho,” alisema Tengeneza.

Licha ya vitambulisho hivyo kutochukuliwa NIDA imesema uzalishaji kupitia mashine mpya zilizofungwa hivi karibuni unaendelea na sasa wanazalisha vitambulisho 1,000 hadi 1,200 kwa saa kutoka vitambulisho 500 vya awali.

error: Content is protected !!