Punyeto/Nyeto/Kujichua ni mojawapo ya njia ambayo mtu hutumia kukidhi mahitaji yake ya kimwili, hasa hitaji la kujamiiana. Njia hii huweza kumpunguzia mtu hamu ya kujamiiana, lakini inaweza kuwa tatizo kubwa kwa kusababisha uraibu kwa mhusika kushindwa kuacha.
Utafiti unaonesha kuwa watu wanaopiga punyeto wanatamani kuacha, kwa kuwa haiwafanyi wajisikie vizuri baada ya tendo hilo. Hizi ni njia sita zinazoweza kumfanya mtu aweze kuacha vitendo vya punyeto.
- Acha kutazama filamu za ngono/picha za utupu
Inaelezwa kuwa filamu za ngono ndio chanzo kikuu cha watu kupiga punyeto. Kwa mtu anayetaka kumaliza tatizo la punyeto kwenye maisha yake, ni lazima aishinde nafsi yake kwa kuacha kutazama filamu/picha za utupu. Sio rahisi kuacha, lakini unaweza kutumia tovuti maalumu zinazochuja maudhui kwenye simu/kompyuta yako kuzuia picha hizo.
- Jitahidi uwe na shughuli za kufanya
Kutokuwa na kazi au shughuli ya kufanya kunaweza kuchochea mtu kupiga punyeto. Hata ikitokea umekosa kazi ya kufanya, jifunze kitu kipya, kama muziki, kuogelea au hata mchezo wowote ambazo utakufanya kutokuwaza kupiga punyeto.
- Tafuta msaada ya kitaalamu
Kuacha Punyeto inaweza kuwa zoezi gumu sana kwa mtu, lakini hii inaweza kuwezekana kupitia waganga wa magonjwa ya akili. Kukutana na mtaalamu wa masuala ya afya ya akili kunaweza kusaidia kwani mtaalamu anaweza kugundua tatizo zaidi linalochochea mtu kupenda punyeto, na akatoa ushauri unaoweza kusaidia.
- Usipende kukaa peke yako
Tabia ya kujitenga inaweza kuwa sababu ya kuanza kupiga punyeto. Faragha binafsi bila kufanya kazi inaweza kuchochea mtu kuendelea kupiga punyeto. Inashauriwa kujichanganya na marafiki au watu wako wa karibu. Kuacha hali ya hii kunaweza kusaidia kupunguza kupiga punyeto tofauti na mtu akikaa peke yake.
- Mazoezi
Mazoezi kama kukimbia, kuogelea na kuruka kamba yanaweza kupunguza tabia ya kupiga punyeto. Mazoezi huzalisha homoni ya ‘endorphins’ ambayo humfanya mtu kujihisi vizuri muda wote. Kuwa na furaha na kujihisi vizuri inapunguza tabia ya kupenda kupiga punyeto mara kwa mara.
- Jiunge na vikundi vya kubadilishana mawazo
Kwa mtu aliyeathirika na kupiga punyeto, anaweza kuacha kwa kupata ushuhuda kutoka kwa mtu aliyefanikiwa kuacha tabia hiyo. Kukutana na watu ambao wamepita tabia kama hiyo, inaweza kumpa mtu mtazamo tofauti na hali yake, na kupata tumaini kuwa anaweza kuacha punyeto.