Paul Makonda kufikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka

HomeKitaifa

Paul Makonda kufikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Taarifa hiyo imeandikwa kwenye gazeti la Raia Mwema toleo la leo (Novemba 15,2021), ambapo inaelezwa kwamba, maombi ya kumfungulia kesi Paul Makonda, yamepelekwa na Mwanasheria wa kujitegemea ambaye jina lake halijawekwa wazi.

Raia Mwema limeeleza kwamba katika Mwanasheria huyo ameomba kibali cha Mahakama kumshitaki Makonda kutokana na makosa anayodaiwa kuyatenda wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kinyume cha Sheria namba 96.

Mwanasheria huyo ameomba Makonda afikishwe kortini pia kujibu tuhuma za kuingilia maudhui ya matangazo ya kituo cha televisheni cha Clouds, alipoenda katika ofisi zao, usiku wa Machi 17,2017.

Paul Makonda alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam tangu mwaka 2016 alipoteuliwa na aliyekuwa Rais wakati huo, Hayati Dkt John Pombe Magufuli. Mwaka 2020 Paul Makonda aliondolewa katika nafasi hiyo ikiwa ni baada ya kutangaza nia ya kugombea Ubunge katika jimbo la Kigamboni.

Iwapo Paul Makonda atafikishwa Mahakamani, atakuwa kiongozi wa pili kukabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka katika kipindi cha hivi karibuni, kwani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya alishafikishwa Mahakamani kwa makosa hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

error: Content is protected !!