PM amsimamisha kazi Mkurugenzi wa jiji Arusha

HomeKitaifa

PM amsimamisha kazi Mkurugenzi wa jiji Arusha

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Mei 24 amewasimamisha kazi watumishi sita wa jiji la Arusha akiwemo Mkurugenzi wa jij hilo Dkt. John Pima kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha na kughushi nyaraka.

Miongoni mwao ni  Mweka Hazina wa Jiji, Mariam Shaban Mshana, Joel Selemani Mtango, Afisa Manunuzi  ambaye alihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Innocent Maduhu (Mchumi), Alex Tlehama (Ofisi ya Mchumi), na Nuru Saqwar (Ofisi ya Mchumi).

“Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ingia kazini mara moja, tafuta nyaraka zote na wakati huo watumishi hawa watakaa pembeni kupisha uchunguzi hadi kazi hiyo itakapokamilika,” amesema na kumuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa afuatilie kujua waliohusika.

Waziri Mkuu amesema hawezi kukaa kimya kuona fedha za umma zikitumika vibaya na kuongeza kuwa Mkurugenzi anatuhumiwa kwa kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na watumishi, matumizi mabaya ya vifaa vya ujenzi wa miradi kutumika kwa ujenzi binafsi ambapo nondo, matofali, misumari, mbao, gypsum boards, saruji, mchanga, kokoto na bati vyenye thamani ya sh. milioni 44 viliagizwa kupitia kampuni ya Cherry General Supplies and Services na kupelekwa kwenye nyumba binafsi iliyoko Olkereyan, eneo la Njiro chini ya Usimamizi wa Mtango.

“Tarehe 28 Machi, 2022 Mkurugenzi ulimwagiza Mweka Hazina aingize shilingi milioni 103 kwenye akaunti binafsi ya Innocent Maduhu iliyoko NMB zikiwa ni masurufu kwa ajili ya shughuli za kiwanda cha matofali. Ni kwa nini fedha ya kazi hii imeingizwa kwenye akaunti ya mtumishi binafsi badala ya akaunti za kata?

“Tarehe 14 Aprili, 2020 uliagiza sh. milioni 65 ziingizwe kwenye akaunti ya Alex Daniel  ya benki ya NMB zikiwa ni malipo kwa ajili ya matenegenezo ya barabara za kata na mitaa. Tarehe hiyohiyo, sh. milioni 65 ziliingizwa kwa Nuru Ginana zikiwa ni malipo ya kununua vifurushi vya moramu. Hapa jumla ni shilingi milioni 233 ambazo hazikutumika kwa lengo lililokusudiwa,” amesema Majaliwa.

Mkurugenzi huyo pia anatuhumiwa kuhamisha watumishi 50 kati ya Januari na Mei mwaka huu.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja, amekagua masoko ya Mbauda, Kilombero na Machame  na kubaini kuwa mabati yaliyotumika kwenye ujenzi wa vibanda vya machinga ni ya geji 30 wakati kanuni zinataka majengo ya Serikali yatumie mabati ya geji 28.

error: Content is protected !!