Pombe ni moja kati ya kinywaji maarufu kinachotumiwa kama kiburudisho na makundi mbalimbali waiwemo vijana na watu wazima.
Hata hivyo, unywaji wa pombe uliopindukia husababisha athari mbalimbali kwa afya ya binadamu ikiwemo magonjwa na vifo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani watu milioni tatu hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi mabaya ya pombe.
Hiyo ni sawa na kusema mtu mmoja hufariki dunia kila baada ya sekunde 10 kutokana na madhara ya pombe ikiwakilisha karibu asilimia tano ya vifo vyote duniania.
WHO inaeleza kuwa asilimia 13.5 ya vifo vyote vinavyotokana na matumizi ya pombe yaliyopitiliza huwapata watu wenye umri wa miaka 20 hadi 39.
“Pombe huwanyang’anya vijana, familia zao na jamii maisha na uwezo wao. Hata hivyo licha ya hatari za wazi kwa afya, udhibiti wa uuzaji wa pombe ni dhaifu sana kuliko bidhaa zingine za uraibu.
“Udhibiti bora, unaotekelezwa vyema na thabiti zaidi wa uuzaji wa pombe ungeokoa na kuboresha maisha ya vijana kote ulimwenguni,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Geneva Uswisi.
WHO imetaja vyanzo mbalimbali vinavyochangia kuongezeka kwa matumizi ya pombe ikiwemo mapinduzi ya kigitali na mbinu zinazotumika katika masoko kukitangaza kinywaji hiki ambapo matangazo mengi hutumia watu maarufu wenye ushawishi kama wanamuzik na wanamitindo.
“Kuongezeka kwa umuhimu wa vyombo vya habari vya kidijitali kunamaanisha kuwa uuzaji wa pombe umezidi kuvuka mipaka”, amesema Dag Rekve kutoka Kitengo cha Pombe, Madawa ya Kulevya na Tabia za Kulevya wa WHO.
Sababu nyingine ya ongezeko hilo ni ushiriki wa makampuni ya vinywaji hivyo katika shughuli za kijamii kama kupinga ukatili, mabonaza, kampeni za usafi, kufadhili ligi za mpira, pamoja na ushirikiano na vilabu, hali inayofanya yajulikane zaidi.
Ili kudhibiti athari za pombe serikali pamoja na wananchi ni lazima wachukue hatua za dhati kudhibiti matumizi yaliyopindukia ya pombe.
Ingawa nchi nyingi zina aina fulani ya sheria za kudhibiti uuzaji wa pombe, bado hazina nguvu.
Katika utafiti wa WHO wa 2018, ilibainika kuwa, wakati nchi nyingi zina aina fulani ya udhibiti wa uuzaji wa pombe katika vyombo vya habari, karibu nusu ya nchi hizo hazina udhibiti wa mtandao (asilimia 48) na mitandao ya kijamii (asilimia 47) ya uuzaji wa pombe.
Ripoti hiyo inahitimisha kwa kuzihimiza serikali za kitaifa kuhakikisha zinajumuisha vikwazo vya kina au marufuku ya uuzaji wa pombe, ikijumuisha vipengele vyake vya kuvuka mpaka ya nchi, katika mikakati yake ya afya ya umma.
Pia zimekumbushwa kuangazia vipengele muhimu na chaguo za udhibiti wa uuzaji wa pombe kuvuka mipaka na kusisitiza haja ya ushirikiano thabiti kati ya mataifa katika eneo hili.
CHANZO: NUKTA HABARI