Rais wa Kenya, William Ruto, amesema kuwa maadui wa mataifa ya Tanzania na Kenya si raia wa nchi hizo bali ni changamoto za kijamii na kiuchumi.
“Maadui wetu sio Wakenya au Watanzania. Maadui wetu ni umaskini, ukosefu wa ajira na maendeleo,” amesema Rais Ruto alipokuwa akilihutubia Bunge la Tanzania.
Ameeleza kuwa Kenya na Tanzania zina utegemezi mkubwa wa kiuchumi, akibainisha kuwa biashara kati ya nchi hizo ilifikia takribani dola bilioni 860 mwaka 2025, huku zikilenga kufikia dola bilioni moja mwaka huu.
“Kenya na Tanzania zinategemeana kwa kiasi kikubwa. Biashara yetu ya pande mbili ilifikia takribani dola bilioni 860 mwaka 2025. Tuko njiani kufikia dola bilioni moja mwaka huu, ishara ya fursa zinazoongezeka, lakini hii bado ni sehemu ndogo tu ya uwezekano uliopo,” amesema.
Aidha, Rais Ruto ametoa wito wa kujitathmini kwa mataifa hayo ili kuhakikisha yanaenda mbele kwa pamoja badala ya kurudia makosa ya zamani.
“Lazima tujiulize kwa uaminifu, je, tunaendelea mbele pamoja au tunarudia makosa ya nyuma? Wakati umefika kwa kizazi chetu kuondoka kwenye hatua ndogo ndogo na kuelekea maendeleo ya pamoja yenye maamuzi thabiti,” ameongeza.


