Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuendelea na ujenzi wa miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa ili kuhakikisha umeme unaozalishwa katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere unawafikia wananchi kote nchini.
Amesema hayo leo Agosti 22, 2026, mkoani Pwani, wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 2,115 wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere.
Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa njia ya umeme ya Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Zuzu mkoani Dodoma.
Rais Samia amesema kukamilika kwa njia hiyo pia kunaiwezesha SGR ya Dodoma kuwa na umeme wake wa uhakika na kuondokana na changamoto ya kuingiliwa kwa umeme unaotumika kuendesha huduma hiyo.
Aidha, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kusambaza umeme nchini, huku akiwataka kuongeza kasi ya kufikisha huduma hiyo kwenye maeneo yaliyosalia.


