Rais Samia ahimiza jamii kuwalea watoto wakike katika maadili mema

HomeKitaifa

Rais Samia ahimiza jamii kuwalea watoto wakike katika maadili mema

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amepongeza mashindano ya dunia ya Qur’an Tukufu kwa wasichana yaliyofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kuwajenga watoto kuwa raia wema na waaminifu.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Rais Samia alisema, “Mashindano haya ni faraja kwa watoto wetu wanaoshiriki na wanaoandaliwa kuwa raia na wazazi wema, kwahiyo ni vema tukaweka nguvu kukuza zaidi mashindano ya aina haya.”

Rais Samia Suluhu akimkabidhi zawadi mshindi wa tano wa Mashindano Makubwa ya Qur’aan kwa Wanawake Duniani Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, Sumaiya Othaman (Tanzania) aliyepata alama ya 93.1.

Rais aliongeza kuwa jitihada za kuendeleza umoja wa kitaifa na kudumisha amani nchini zinachangia katika heshima na kukubalika kwa Tanzania kimataifa. Aliwasihi Watanzania waendelee kulinda amani ya nchi kwa kusema, “Kukubalika kwetu pamoja na rehema za Mwenyezi Mungu, ni kutokana na jitihada zetu za kuendeleza umoja wa kitaifa na kudumisha amani nchini kwetu, hivyo niwasihi Watanzania wenzangu, tuendelee kuilinda heshima hii kwa kudumisha amani nchini kwetu.”

Katika hotuba yake, Rais Samia pia alizungumzia umuhimu wa kumlea mtoto wa kike katika misingi ya kiimani na maadili, akibainisha kuwa, “Kumlea mtoto wa kike katika misingi mizuri ya kiimani unakuwa unaandaa mwanamke au mama atakayeishi katika misingi hiyo. Mtakubaliana nami kuwa watu wazima wenye imani na wenye misingi ya uadilifu na kutenda haki, kwa kiasi kikubwa ni zao la misingi imara waliyopitia katika ngazi za makuzi yao ndani ya familia zao.”

Rais Samia alihitimisha hotuba yake kwa kutoa wito wa kuendelea kuwekeza katika maadili na kuandaa kizazi kijacho kuwa raia wenye mchango chanya kwa jamii.

error: Content is protected !!