Soma hapa maagizo 7 yaliyotolewa na Rais Samia leo

HomeKitaifa

Soma hapa maagizo 7 yaliyotolewa na Rais Samia leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua kampeni ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Katika hotuba yake aliyoitoa leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dodoma, ametoa maagizo mahsusi kwa wale wote watakaohusika katika utekelezaji wa mpango huo.

Baadhi ya maagizo hayo ni;

Jambo la kwanza aliloagiza Rais Samia Suluhu ni kutumika zaidi kwa wakandarasi wa ndani, ili kuhakikisha kwamba fedha zinazotumika katika mpango huu zinabaki katika mzunguko wa fedha nchini.

Agizo la pili ni kwamba utaratibu wa manunuzi wa ‘single source’ utumike katika ujenzi na ununuzi wa vifaa. Amesema utaratibu huo utaharakisha upatikanaji wa vifaa na kukamilika haraka kwa ujenzi, tofauti na utaratibu wa kawaida wa manunuzi ambao huchukua muda mrefu zaidi.

Tatu, amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango kuharakisha misamaha ya kodi katika vifaa na bidhaa zitakazoingizwa nchini kwa ajili ya mpango huu.

Nne, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameagizwa kukagua matumizi ya fedha zote zitakazotumika katika mpango huo. Rais Samia amemtaka CAG pamoja na Mkaguzi wa Ndani, kuhakikisha wanafuatilia matumizi yote na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi yote.

Tano, Rais Samia pia ameungana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kuziagiza Kamati za Bunge kwenda kutembelea miradi na kusimamia matumizi ya fedha hizo.

Sita, Agizo lingine alilolitoa Rais Samia Suluhu ni kuundwa kwa kamati katika mikoa, huku akitoa angalizo kwamba hataki utitiri wa kamati. “Kumeshaonekana kuna fedha hapa, kutakuwa na utitiri wa kamati, sitaki utitiri wa kamati,” amesema Rais Samia.

Saba, Rais Samia ameagiza kuwepo kwa nidhamu katika matumizi ya fedha za mpango huo. Alitoa agizo hilo sambamba na onyo kali kwamba hatakuwa na huruma kwa wale watakaofanya ubadhilifu.

“Kwa wale wanaotaka kuzijua rangi zangu halisi, wajaribu kudokoa fedha hizi au wabadilishe matumizi ya fedha hizi bila maelewano,” amesisitiza Rais Samia Suluhu.

Mpango huo wa Ustawi wa Taifa na Mapambano didhi ya UVIKO-19 utarajiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miezi tisa.

error: Content is protected !!