Elon Musk asita

HomeKimataifa

Elon Musk asita

Bilionea Elon Musk amesema amesitisha kwa muda mchakato wa ununuzi mtandao wa Twitter wenye thamani ya Dola za Marekani  bilioni 44 (Sh102.3 trilioni) hadi apate maelezo zaidi kuhusu akaunti feki kwenye jukwaa hilo.

​Hata hivyo, Musk anayemiliki kampuni ya magari ya umeme ya Tesla anaendelea kukutana na viongozi wa juu wa Twitter kwa siku tatu kujadili biashara yake kabla ya kutangaza hadharani kuhusu ununuzi huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kuwa mtandao huo una akaunti feki za watumiaji ambazo anaamini zinaweza kuleta changamoto katika matangazo kwa sababu siyo watu halisi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, Musk amependekeza akaunti hizo zipunguzwe hadi asilimia 5 ya watumiaji wote ili aweze kuendelea na mpango wake wa kuinunua Twitter.

Haya yalijitokeza mwishoni mwa Machi na mapema Aprili wakati Musk alipofanya mazungumzo na mwanzilishi mwenza wa Twitter na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani Jack Dorsey, Mkurugenzi Mtendaji wa sasa Parag Agrawal, Mwenyekiti wa Bodi ya Twitter Bret Taylor na mjumbe wa bodi Egon Durban na watendaji wengine wa kampuni.

Baada ya mazungumzo hayo Bodi ya Twitter ilikubali kumuuzia Musk kwa Sh102.3 trilioni mwishoni mwa mwezi uliopita,  lakini ununuzi huo hautasonga mbele hadi Musk awe na ufahamu wa wazi wa idadi ya akaunti feki kwenye jukwaa hilo.

Katika mkutano wa teknolojia uliofanyika Miami, Marekani Mei 16, 2022 Musk alikadiria kuwa takriban asilimia 20 ya akaunti milioni 229 za Twitter ni feki.

SOURCES : NUKTA HABARI

error: Content is protected !!