Rais Samia ahimiza uhifadhi wa chakula

HomeKitaifa

Rais Samia ahimiza uhifadhi wa chakula

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutouza nje ya nchi chakula chote kinachovunwa bali kihifadhiwe kwa ajili ya kuongeza akiba itakayosaidia kukabiliana na upungufu wa chakula unaoikabili dunia kwa sasa.

Rais Samia, aliyekuwa akishiriki uzinduzi wa tamasha la utamaduni la Bulabo jana Juni 13, 2023 jijini Mwanza, amewaambia Watanzania kuwa kutokana na athari za Uviko-19, mabadiliko ya tabia nchi na vita ya Urusi na Ukraine ulimwengu unatarajiwa kuwa na uhaba mkubwa wa chakula.

“Sababu hizi ambazo zimekuwepo kwa miaka mitatu, minne mfululizo zimefanya nchi zetu haziwezi kuzalisha chakula cha kutosha, na kule kwenye chakula kuna vikwazo hivyo hakiwezi kwenda sehemu nyingine za dunia,” amesema Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia upungufu wa chakula unachochea mfumuko wa bei katika maeneo mbalimbali duniani ambapo kwa sasa unaanzia asilimia 10 na kuendelea, na Serikali yake imekuwa ikichukua hatua kadhaa kukabiliana nao ikiwemo kutoa ruzuku kwenye mafuta na mbolea.

Ili kukabiliana na upungufu wa chakula nchini Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo, kuongeza uwezo wa maghala ya kuhifadhi chakula pamoja na ujenzi wa skimu za kilimo zitakazosaidia kilimo kufanyika kwa misimu miwili jambo litakalo ongeza mavuno.

“Nimeshatoa kibali kwa Waziri wa Kilimo washirikiane na Waziri wa Fedha kutoa fedha kwa ajili ya kununua tani 500 za chakula, matarajio yetu kwa Serikali tani moja iwe inatumiwa na watu 20 kuliko ilivyo sasa ambapo tani moja inategemewa na watu 180,” amesema Rais Samia.

Mazingira, utamaduni vilindwe

Rais Samia ametumia fursa hiyo ya uzinduzi wa sherehe za mwanzo wa msimu wa mavuno kuwaagiza Machifu kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi mazingira pamoja na kuwalea vijana katika kutunza maadili ya kitanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pindi Chana amesema Serikali ina wajibu wa kulinda na kuenzi tamaduni za asili pamoja na kutunza tamaduni kwa kuwa ni  chanzo kizuri cha mapato.

Waziri Chana amevitaka vikundi vya sanaa na utamaduni kujisajiri ili vitambulike rasmi kupitia ofisi za maofisa utamaduni wa wilaya au kupitia tovuti ya ya wizara hiyo ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo mikopo.

error: Content is protected !!